Breaking News


 Jiji la Dar es Salaam lilianza kama Kijiji kidogo cha wavuvi kilichojulikana kama Mzizima. Kijiji hiki kilianzishwa na Wabalawa ambao walichanganyika na Wazaramo kuelekea kwenye maeneo ya Bara la Afrika Mashariki na ambazo zilijulikana kama ‘Caravan Routes’. Ujenzi wa Makao ya Sultani pamoja na bandari ulianza rasmi mwaka 1865 katika eneo la kijiji cha Mzizima. Ujenzi huo ulikamilika mwaka 1866 na Sultani Majid bin Said kuhamia Dar es Salaam mwaka huo.

Mara baada ya Sultani Majid bin Said kuhamia Dar es Salaam mji ulianza kupanuka na uchumi wake kukua kwa kasi kubwa japo kwa kipindi kifupi ambapo Sultani Majid bin Said alifariki mwaka 1870. Kifo cha Sultani huyo kilisababisha kudidimia kwa maendeleo ya mji wa Dar es Salaam. Hali hiyo ilianza tena kubadilika mwaka 1884 kufuatia kuanzishwa kwa koloni la Wajerumani la Afrika Mashariki. Mwaka 1891

Serikali ya kikoloni ya Kijerumani iliamua kuhamisha makao makuu ya utawala wake katika Afrika Mashariki kutoka Bagamoyo na kuyaweka Dar es Salaam. Hata hivyo, baada ya Wajerumani kushindwa na Waingereza katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1916, Mji wa Dar es Salaam uliendelea kuwa makao makuu ya utawala wa koloni la Waingereza nchini Tanganyika hadi ilipojipatia uhuru wake mwaka 1961. Dar es Salaam iliendelea kuwa makao makuu ya Tanganyika huru na hatimaye kuwa makao makuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi mwaka 1972 wakati Serikali ilipoamua kuhamishia makao yake makuu mjini Dodoma. Jiji la Dar es Salaam liliendelea kubaki kuwa maarufu kwa kuwa Jiji kuu na kitovu cha biashara nchini Tanzania.

Hadhi ya Mji, Manispaa na Jiji

Mji wa Dar es Salaam ulitangazwa kuwa Mji wenye Serikali yake ya Mitaa mwaka 1920. Hadhi ya Mji wa Dar es Salaam ilipandishwa kuwa ya Manispaa mwaka 1949 nabaadaye kutunukiwa hadhi ya Jiji na Malkia wa Himaya ya Uingereza tarehe 10 Desemba 1961 mara baada ya Tanganyika kupata uhuru wake. Kuanzia kipindi hicho, Jiji la Dar es Salaam lilikuwa likiongozwa na Halmashauri ya Jiji hadi mwaka 1972 wakati ambapo Serikali ilivunja Serikali zote za Mitaa nchini ili kutekeleza mfumo wa madaraka Mikoni. Mamlaka za Miji zilirejeshewa madaraka mwaka 1978 ambapo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam lilianza kufanya kazi tena.

Serikali za Mitaa

Kabla ya Ukoloni walitawala Machifu na Wazee wa mila. Wakati wa Utawala wa Wajerumani (1884-1917) utawala wa kikoloni ulikuwa wa moja kwa moja zaidi maeneo ya mijini “Direct rule”. Katika kipindi cha utawala wa Waingereza (1917-1961) katika mwaka 1926 kulikuwa na utawala wa kikabila. Sheria ya Serikali za Mitaa zilianza mwaka 1953 na Sheria ya Miji mwaka 1946. Baada ya mwaka 1961 uliondolewa Utawala wa Machifu na kuanza Mfumo wa pamoja wa Serikali za Mitaa. Mwaka 1972 Serikali za Mitaa ziliondolewa na kuanza Utawala Mijini na mwaka 1982 Sheria ya Serikali za Mitaa zilirejeshwa tena. Mwaka 1984 ulirejeshwa mfumo wa Serikali za Mitaa na kudumu hadi mwaka 1995. Mpango wa uboreshaji wa Serikali za Mitaa kuzifanya ziwe na uwezo wa utendaji, uwazi na uwajibikaji ulianzishwa mwaka 1996 uliojulikana kama “Local Government Reform Programme”.

Mkoa wa Dar es Salaam wenye eneo na km za mraba 1,800 ulianzishwa kutoka Mkoa wa Pwani mwaka 1973 ukiwa na Wilaya 3 za Ilala, Kinondoni na Temeke. Mamlaka za Serikali za Mitaa za Mkoa wa Dar es Salaam zilizopo sasa zilianzishwa mwaka 2000 baada ya kuvunjwa kwa Tume ya Jiji iliyokuwepo kufuatia kuvunjwa kwa Serikali za Mitaa mwaka 1996 kulikoendelea hadi mwishoni mwa mwaka 1999.

Post a Comment

Previous Post Next Post
Contact ME
close